Sunday 3 April 2011

*TWAREJESHWA JEHANAMU?* Wakati manabii wa ukweli na watetezi wa haki walipoipiga baragumu kwa Wakenya dhidi ya kuipitisha katiba iliyouficha ndani mfumo wa majimbo,walikejeliwa,wakaitwa wasaliti,wahafidhina na vipofu wasioona mbele. Walitengwa na jamii nzima ya Wakenya na ni wachache tu walizozisikiliza tabiri na maonyo yao dhidi ya kujitia kitanzi kwa kuunga mkono mfumo wa majimbo ambao ni mhimili dhabiti wa utawala wa ukoloni ulioyatenganisha makabila mbalimbali hapa nchini ili uweze kuupora utajiri wa kiraslimali wa nchi hii bila upinzani wa pamoja wa jamii hizi.Wakoloni walitumia mfumo wa tenga-tawala ili kuweza kuyahadaa makabila mbalimbali kuwashambulia wenzao ili kuweza kunufaika kiraslimali. Majimbo haya yanayoitwa 'kaunti' ili kutoonekana machoni mwa wengi kama majimbo ni saratani ya kiutawala tuliyojiwekea sisi wenyewe pamoja na vizazi vijavyo kwa karne nyingi zitakazokuja.Ni kosa ambalo dawa yake mujarabu haiwezi ikapatikana kiurahisi. Muungano wa kikabila unaowashirikisha Wakikuyu,Wakamba na Wakalenjin ni mwanzo tu wa vilio na kusaga meno kwa makosa tuliyoyafanya.Huku ikizingatiwa kwamba majimbo haya tayari yamegawika kwa misingi ya kikabila ambapo Wakikuyu wamepewa himaya yao,Wakalenjin vile vile,Wakamba,Wajaluo,Wakisii na kadhalika,lile tumefanyani kuibua upya dhana d za chuki za kikabila miongoni mwa jamii hizi baada ya kuipitisha katiba hii. Wakikuyu katika eneo la Mlima Kenya au Kati mwa nchi wana dhana ya kwamba hili ni eneo lao na wengine ni wageni.Waluo katika eneo la Nyanza vile vile wana dhana iyo hiyo.Makabila yote arobaini na mawili yakiwa na dhana kama hizi basi itakuwa vigumu sana kwa jamii hizi kutangamana pamoja,kuishi,kuyanunua mashamba,kufanya biashara au hata kuyatembelea maeneo ya jamii nyengine nchini kwani kwa misingi na falsafa ya nchi iliyogawika kimajimbo,ataonekana kama 'mgeni' na adui asiyestahili kamwe kuwepo katika eneo hilo.Mkalenjin anapotembelea katika eneo la Mlima Kenya,ataonekana kama ni raia wa nchi ngeni,hivyo basi atahisi kwamba kamwe hafai kuwepo wala kuwa na uhusiano wowote ule na wakaazi wa eneo hilo,iwe,kijamii,kisiasa au kiuchumi. Ikiwa hivi ndivyo itakavyokuwa,basi ni kwa nini machafuko mengine ya kikabila yasitokee hata mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita(ICC)inapopania kuwashtaki watuhumiwa wakuu wa ghasia za 2007 na tushajijengea Jehanamu tayari kwa kuukumbatia mfumo wa majimbo na kuyatupilia mbali maonyo na tabiri za watetezi wa haki na manabii wa ukweli? Nani asiyekumbuka juhudi za vuguvugu la Kadi Nyekundu lilililowashirikisha Waheshimiwa Koigi wa Wamwere,Njeru Kathangu,Wanyiri Kihoro miongoni mwa wanaharakati wengine?Vuguvugu hili lilifanya mikutano mbalimbali na kuwaonya Wakenya dhidi ya kuingia ndege inayoonesha wekundu wa moto ambapo baadaye ingelipukia hewani?Wengi waliamua kufuata upofu wa wimbi la ukabila.Waliipitisha katiba hiyo kwa sababu viongozi wao wa kijamii na kisiasa waliiunga mkono. Waliamua kutozisaliti jamii zao hivyo basi kufanya uamuzi ambao wao wenyewe hawakujua hatima yake.Kuna wale walioujua ukweli lakini wakaamua kuudumisha uzalendo wa kikabila ili kutoonekana wasaliti wakuu wa jamii zao. Mabwanyenye,mafisadi wa mibabe wa ukabila waliowachochea Wakenya kuuana,kuwachomea makao,kuwabaka na kuwafurusha kutoka makao yao hutumia usahaulifu wa Wakenya kama daraja kuu ya kuwapumbaza ili kujitakia makuu.Hili ndili dhihirisho la Muungano wa KKK.Wawili wa viongozi hawa ni watuhumiwa wa uchochezi wa mauaji,ubakaji na uporaji wakuu wa utajiri wa taifa hili. Kana kwamba Wakenya hawajifunzi na wanayoyapitia au waliyoyapitia,tayari washasahau athari za ghasia za 2007/2008 japo makovu wa athari hizi yangali machoni mwetu,kama vile wahanga wa machafuko haya,ambao bado wamo makambini wanakokufia na kutesekea kwani jamii pana ya Wakenya na hata serikali imewasahau kwa ahadi zisizotimia za kuwatafutia mashamba au makao mbadala. Japo ni ghasia zilizopangwa kabla ya uchaguzi mkuu,ndani yake kuna chocheo la tofauti za kisiasa ambacho ndicho kilikuwa kiini hasa cha ubakaji,uporaji an mauaji yaliyofanywa dhidi ya Wakenya ambao hawakuwa na hatia yoyote kuuawa au kuteketezwa wakiwa hai mbali hatia yao kuu ilikuwa kuwa aidha kuwa Wakikuyu,Waluo,Wakisii au jamii nyingine.Baada ya hatia hii ya kimaumbile,adhabu yao ilikuwa ni kuuawa kinyama na kubakwa ili kuzitosheleza hasira za mibabe hawa wa kikabila.Hili linaiafiki methali isemayo kwamba 'wapiganao fahali wawili,nyasi ndizo huumia.' Mnamo 2002,baada ya Muungano wa NARC kuung'atua utawala wa KANU,tulifumbwa macho kwamba huu ulikuwa muungano wa viongozi walioongozwa na falsafa ya utaifa.Tulisahau kwamba huu ulikuwa muungano wa mafisadi na manyapaa ambao ili kuzitimiza ndoto zao za kisiasa sharti wangeungana ili kuwapumbaza Wakenya wasahaulifu. Ndani ya muungano huu ukabila,wivu na kujitakia makuu uliwaingia baadhi ya mibabe hawa na ukabila na kuwasaliti wenzao kwa kutozingatia mikataba ya kugawana mamlaka na ndipo chombo kikaanza kuyumbayumba katikati mwa bahari lenye mawimbi. Ni hapa ambapo Waziri Mkuu Raila Odinga alijitenga na Rais Kibaki baada ya katiba iliyopendekezwa kufeli kushughulikia mikataba yao kwamba Raila Odinga angekuwa waziri mkuu mwenye mamlaka pindi tu baada ya Wakenya kuipitisha katiba hiyo. Ni hili lililosababisha uasi wa Raila na waandani wake ambapo walitemwa kutoka baraza la mawaziri lililofanyiwa mageuzi makubwa baada ya mlengo wa 'ndiyo' wa Rais Kibaki kushindwa vibaya katika kura ya maamuzi ya tarehe 27 Novemba 2005.Mvutano huu ambao uliligawanya taifa hili katika makundi mawili ndiyo ulikuwa chanzo kikuu cha machafuko ya 2007/2008,nchi ilipowaka moto na ikabidi jumuiya ya kimataifa kuingilia kati ili kuzima makali yake kwa wana wa taifa hili. Taharuki iliyozuka tangu Novemba 27 2005,ambapo bila shaka viongozi pamwe na makabila yao walidhani kwamba Rais Kibaki,chini ya ushawishi wa vyombo vya dola angefanya kila awezalo ili kushinda uchaguzi wa 2007,sharti wangefanya mikakati mwafaka ili kujitetea 'kupata haki' ambapo ilikuwa ni kufadhili mashambulizi dhidi ya wafuasi wa mlengo wa PNU. Naam,taharuki hii ya kisiasa iliyotanda na kutamalaki nchini tangu matokeo ya kura ya maoni ya tarehe 27 Novemba 2007,ndiyo iliyolipuka na matokeo yake yakawa ni machafuko ya kikabila ambayo nusura yaliingize taifa hili katika lindi la mauaji ya kimbali kama ya Rwanda mnamo 1994. Na kama vile tumeshuhudia tangu enzi za Mzee Jomo Kenyatta,miungano ya kisiasa ambayo ndani yake huficha saratani ya ukabila huwa nyenzo ya makuu ya kisiasa kwa viongozi wetu lakini laana kwa wananchi wanaowaabudu mibabe hawa wa ukabila kwa upofu bila kujua madhara ya utengano wakati mabishano yanapotokea katika kuisherehekea 'nyama' wanayoipata baada ya kuwapumbaza wananchi. Tofauti za Rais Kenyatta na Oginga Odinga ndizo zilizopelekea kuwepo kwa uhasama wa kisiasa kati ya jamii za Wakikuyu na Waluo kwa miongo minne ambapo uhasimu huu hauishi hivi karibuni kwani mbegu ya chuki za kikabila iliyopandwa na viongozi hawa imezidi kuzagaa kando kupasishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine huku nchi ikiendelea kuiabudu miungano ya kisiasa na kikabila na vibaya zaidi,kujitia kitanzi cha kuipitisha katiba iliyojaa mapungufu kama mfumo wa majimbo uliofichika kwa kupewa majina kama vile 'ugatuzi', 'kaunti' na kadhalika ambao unaendeleza utengano wa kikabila. Vile vile alipochukua hatamu za uongozi,Rais Daniel arap Moi aliufuata mkondo ule ule wa mtangulizi wake.Kwa mfano,aliwaangusha na kuwang'atua viongozi wengi Wakikuyu waliokuwa wamelelewa na kutunzwa na utawala wa Kenyatta hivyo basi ikawa ni zamu yake na jamii ya Wakalenjin pamwe na wandani waliomwabudu kujikuza na kusherehekea matunda ya utajiri wa nchi. Mfumo huu wa Moi uliwafanya Wakikuyu kuwa pembezoni mwa ulingo wa kisiasa na uongozi wa kitaifa uliozingatia mtindo wa kuwatunza wazalendo wa utawala huo. Chuki hii iliendelea kuwa mbaya zaidi baada ya Moi shingo upande kukubali kuifanya nchi kuwa na uhuru wa kisiasa mnamo 1992,baada ya kushinikizwa na mashirika ya umma,jumuiya ya kimataifa,watu binafsi kama vile mawakili,waandishi wa habari na wakereketwa wa mapinduzi ya kweli.Mfumo huu aidha uliifanya nchi kuziabudu siasa kwa misingi ya kikabila huku mbegu ya chuki za kikabila iliyopandwa na Kenyatta na Moi ikizidi kuyastawisha matawi yake hadi 2007 ambapo upeo wa athari ulionekana-jamii zikishambuliana zenyewe. Vivo hivo,viongozi tuliyo nao hivi sasa kama vile Kalonzo Musyoka,Uhuru Kenyatta na William Ruto wanaopania kuwania urais mnamo 2012 ni wanafunzi wa kisiasa wa marais waliotangulia na kwa hivyo,mtindo ni ule ule wa 'walimu wao wa kisiasa' utatumika hasa wanaposisitiza kubuni muungano wa kikabila unaowashirikisha Wakikuyu,Wakalenjin na Wakamba. Lakini kama kawaida,tumejitia upofu na kushangilia wanapoturejesha kwenye Jehanamu iwakayo moto lakini tumegubikwa na hamnazo kuu. Manabii wanazidi kubasihri kwamba,litakalotokea litakuwa ni gharika la kisiasa ambalo huenda likawasomba waliobaki,mashamba yao,wana waliozaliwa na damu zao kuzoleka mchangani zisiweze kurudi wala kuonekana tena.Tunajifanya hatujui madhara ya miungano ya kikabila hasa inapovunjika. Damu na roho za waliochinjwa na kuchomwa wakiwa uhai zinazidi kulia katika wafu,huku zikidai na kulilia haki.Haki ya hukumu itendeke kwa wale waliohitimisha mioyo ya wana hawa wa Mungu wasio na makosa hapa duniani kupitia madhila waliyopitia,siku yao ikiwa haijatimia. Haki itendeke kwa wanaotesekea kambini kwa miaka minne sasa huku waliowaua,kuwachinja kama wanyama,kuwabaka na kuwafurusha kutoka mashamba yao wakizidi kuachiliwa kwa ukosefu wa ushahidi. Ndimi za wahanga hawa zimechoka kwa kulilia haki.Sauti zao zimefifia kwa ukosefu wa nguvu ya kulilia haki yao kutokana na njaa,utapiamlo pamwe na baridi shadidi ya usiku ambayo hupenya ndani kwa ndani mle hemani zilizochanikachanika kwa kuangaziwa na jua pamoja na kunyeshewa na mvua kwa muda wa miaka miine. Kipindipindu kimeyachukua maisha yao kutokana na mafuriko yanayowakumba mara kwa mara na kuzisomba hema na kambi zao. Kwa sasa,wamechoka kudai haki kwa kwa manyapaa wasiojali ambao wakati huu wanabuni daraja za kubakia madarakani mnamo 2012,wakiwashajiisha wahanga hawa kuyasahau yaliyopita na kuwaunga mkono katika miungano hii ya kikabila. Na kuonyesha kiwango cha usahaulifu wa kutojali kwa viongozi hawa,wameamua kuzifuja fedha ambazo zingewasitiri wahanga hawa,angaa kuwasahalisha kwa muda njaa,baridi,maradhi na fikra za unyama walioushuhudia ukitendwa dhidi ya wenzao miaka minne iliyopita. Ni mzinduko pekee wa kimawazo,kuzisikiza nyaadhi za manabii wa ukweli zitatunusuru kutoka kwa madhara haya ya ufurukutwa wa ukabila. Hivyo basi,juhudi za Rais Mwai Kibaki kuleta uwiano na maridhiano miongoni mwa Wakikuyu na Wakalenjin mkoani Bonde la Ufa,huenda ukawa na athari za muda mfupi tu kwani unafungamanishwa na kufaulu kumpa upinzani Waziri Mkuu Raila Odinga mnamo 2012,japo makabila haya mawili bado yanaweza yakajitanzua kutoka kwa historia mbaya ya uhasama kati yao.*TWAREJESHWA JEHANAMU?* Wakati manabii wa ukweli na watetezi wa haki walipoipiga baragumu kwa Wakenya dhidi ya kuipitisha katiba iliyouficha ndani mfumo wa majimbo,walikejeliwa,wakaitwa wasaliti,wahafidhina na vipofu wasioona mbele. Walitengwa na jamii nzima ya Wakenya na ni wachache tu walizozisikiliza tabiri na maonyo yao dhidi ya kujitia kitanzi kwa kuunga mkono mfumo wa majimbo ambao ni mhimili dhabiti wa utawala wa ukoloni ulioyatenganisha makabila mbalimbali hapa nchini ili uweze kuupora utajiri wa kiraslimali wa nchi hii bila upinzani wa pamoja wa jamii hizi.Wakoloni walitumia mfumo wa tenga-tawala ili kuweza kuyahadaa makabila mbalimbali kuwashambulia wenzao ili kuweza kunufaika kiraslimali. Majimbo haya yanayoitwa 'kaunti' ili kutoonekana machoni mwa wengi kama majimbo ni saratani ya kiutawala tuliyojiwekea sisi wenyewe pamoja na vizazi vijavyo kwa karne nyingi zitakazokuja.Ni kosa ambalo dawa yake mujarabu haiwezi ikapatikana kiurahisi. Muungano wa kikabila unaowashirikisha Wakikuyu,Wakamba na Wakalenjin ni mwanzo tu wa vilio na kusaga meno kwa makosa tuliyoyafanya.Huku ikizingatiwa kwamba majimbo haya tayari yamegawika kwa misingi ya kikabila ambapo Wakikuyu wamepewa himaya yao,Wakalenjin vile vile,Wakamba,Wajaluo,Wakisii na kadhalika,lile tumefanyani kuibua upya dhana d za chuki za kikabila miongoni mwa jamii hizi baada ya kuipitisha katiba hii. Wakikuyu katika eneo la Mlima Kenya au Kati mwa nchi wana dhana ya kwamba hili ni eneo lao na wengine ni wageni.Waluo katika eneo la Nyanza vile vile wana dhana iyo hiyo.Makabila yote arobaini na mawili yakiwa na dhana kama hizi basi itakuwa vigumu sana kwa jamii hizi kutangamana pamoja,kuishi,kuyanunua mashamba,kufanya biashara au hata kuyatembelea maeneo ya jamii nyengine nchini kwani kwa misingi na falsafa ya nchi iliyogawika kimajimbo,ataonekana kama 'mgeni' na adui asiyestahili kamwe kuwepo katika eneo hilo.Mkalenjin anapotembelea katika eneo la Mlima Kenya,ataonekana kama ni raia wa nchi ngeni,hivyo basi atahisi kwamba kamwe hafai kuwepo wala kuwa na uhusiano wowote ule na wakaazi wa eneo hilo,iwe,kijamii,kisiasa au kiuchumi. Ikiwa hivi ndivyo itakavyokuwa,basi ni kwa nini machafuko mengine ya kikabila yasitokee hata mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita(ICC)inapopania kuwashtaki watuhumiwa wakuu wa ghasia za 2007 na tushajijengea Jehanamu tayari kwa kuukumbatia mfumo wa majimbo na kuyatupilia mbali maonyo na tabiri za watetezi wa haki na manabii wa ukweli? Nani asiyekumbuka juhudi za vuguvugu la Kadi Nyekundu lilililowashirikisha Waheshimiwa Koigi wa Wamwere,Njeru Kathangu,Wanyiri Kihoro miongoni mwa wanaharakati wengine?Vuguvugu hili lilifanya mikutano mbalimbali na kuwaonya Wakenya dhidi ya kuingia ndege inayoonesha wekundu wa moto ambapo baadaye ingelipukia hewani?Wengi waliamua kufuata upofu wa wimbi la ukabila.Waliipitisha katiba hiyo kwa sababu viongozi wao wa kijamii na kisiasa waliiunga mkono. Waliamua kutozisaliti jamii zao hivyo basi kufanya uamuzi ambao wao wenyewe hawakujua hatima yake.Kuna wale walioujua ukweli lakini wakaamua kuudumisha uzalendo wa kikabila ili kutoonekana wasaliti wakuu wa jamii zao. Mabwanyenye,mafisadi wa mibabe wa ukabila waliowachochea Wakenya kuuana,kuwachomea makao,kuwabaka na kuwafurusha kutoka makao yao hutumia usahaulifu wa Wakenya kama daraja kuu ya kuwapumbaza ili kujitakia makuu.Hili ndili dhihirisho la Muungano wa KKK.Wawili wa viongozi hawa ni watuhumiwa wa uchochezi wa mauaji,ubakaji na uporaji wakuu wa utajiri wa taifa hili. Kana kwamba Wakenya hawajifunzi na wanayoyapitia au waliyoyapitia,tayari washasahau athari za ghasia za 2007/2008 japo makovu wa athari hizi yangali machoni mwetu,kama vile wahanga wa machafuko haya,ambao bado wamo makambini wanakokufia na kutesekea kwani jamii pana ya Wakenya na hata serikali imewasahau kwa ahadi zisizotimia za kuwatafutia mashamba au makao mbadala. Japo ni ghasia zilizopangwa kabla ya uchaguzi mkuu,ndani yake kuna chocheo la tofauti za kisiasa ambacho ndicho kilikuwa kiini hasa cha ubakaji,uporaji an mauaji yaliyofanywa dhidi ya Wakenya ambao hawakuwa na hatia yoyote kuuawa au kuteketezwa wakiwa hai mbali hatia yao kuu ilikuwa kuwa aidha kuwa Wakikuyu,Waluo,Wakisii au jamii nyingine.Baada ya hatia hii ya kimaumbile,adhabu yao ilikuwa ni kuuawa kinyama na kubakwa ili kuzitosheleza hasira za mibabe hawa wa kikabila.Hili linaiafiki methali isemayo kwamba 'wapiganao fahali wawili,nyasi ndizo huumia.' Mnamo 2002,baada ya Muungano wa NARC kuung'atua utawala wa KANU,tulifumbwa macho kwamba huu ulikuwa muungano wa viongozi walioongozwa na falsafa ya utaifa.Tulisahau kwamba huu ulikuwa muungano wa mafisadi na manyapaa ambao ili kuzitimiza ndoto zao za kisiasa sharti wangeungana ili kuwapumbaza Wakenya wasahaulifu. Ndani ya muungano huu ukabila,wivu na kujitakia makuu uliwaingia baadhi ya mibabe hawa na ukabila na kuwasaliti wenzao kwa kutozingatia mikataba ya kugawana mamlaka na ndipo chombo kikaanza kuyumbayumba katikati mwa bahari lenye mawimbi. Ni hapa ambapo Waziri Mkuu Raila Odinga alijitenga na Rais Kibaki baada ya katiba iliyopendekezwa kufeli kushughulikia mikataba yao kwamba Raila Odinga angekuwa waziri mkuu mwenye mamlaka pindi tu baada ya Wakenya kuipitisha katiba hiyo. Ni hili lililosababisha uasi wa Raila na waandani wake ambapo walitemwa kutoka baraza la mawaziri lililofanyiwa mageuzi makubwa baada ya mlengo wa 'ndiyo' wa Rais Kibaki kushindwa vibaya katika kura ya maamuzi ya tarehe 27 Novemba 2005.Mvutano huu ambao uliligawanya taifa hili katika makundi mawili ndiyo ulikuwa chanzo kikuu cha machafuko ya 2007/2008,nchi ilipowaka moto na ikabidi jumuiya ya kimataifa kuingilia kati ili kuzima makali yake kwa wana wa taifa hili. Taharuki iliyozuka tangu Novemba 27 2005,ambapo bila shaka viongozi pamwe na makabila yao walidhani kwamba Rais Kibaki,chini ya ushawishi wa vyombo vya dola angefanya kila awezalo ili kushinda uchaguzi wa 2007,sharti wangefanya mikakati mwafaka ili kujitetea 'kupata haki' ambapo ilikuwa ni kufadhili mashambulizi dhidi ya wafuasi wa mlengo wa PNU. Naam,taharuki hii ya kisiasa iliyotanda na kutamalaki nchini tangu matokeo ya kura ya maoni ya tarehe 27 Novemba 2007,ndiyo iliyolipuka na matokeo yake yakawa ni machafuko ya kikabila ambayo nusura yaliingize taifa hili katika lindi la mauaji ya kimbali kama ya Rwanda mnamo 1994. Na kama vile tumeshuhudia tangu enzi za Mzee Jomo Kenyatta,miungano ya kisiasa ambayo ndani yake huficha saratani ya ukabila huwa nyenzo ya makuu ya kisiasa kwa viongozi wetu lakini laana kwa wananchi wanaowaabudu mibabe hawa wa ukabila kwa upofu bila kujua madhara ya utengano wakati mabishano yanapotokea katika kuisherehekea 'nyama' wanayoipata baada ya kuwapumbaza wananchi. Tofauti za Rais Kenyatta na Oginga Odinga ndizo zilizopelekea kuwepo kwa uhasama wa kisiasa kati ya jamii za Wakikuyu na Waluo kwa miongo minne ambapo uhasimu huu hauishi hivi karibuni kwani mbegu ya chuki za kikabila iliyopandwa na viongozi hawa imezidi kuzagaa kando kupasishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine huku nchi ikiendelea kuiabudu miungano ya kisiasa na kikabila na vibaya zaidi,kujitia kitanzi cha kuipitisha katiba iliyojaa mapungufu kama mfumo wa majimbo uliofichika kwa kupewa majina kama vile 'ugatuzi', 'kaunti' na kadhalika ambao unaendeleza utengano wa kikabila. Vile vile alipochukua hatamu za uongozi,Rais Daniel arap Moi aliufuata mkondo ule ule wa mtangulizi wake.Kwa mfano,aliwaangusha na kuwang'atua viongozi wengi Wakikuyu waliokuwa wamelelewa na kutunzwa na utawala wa Kenyatta hivyo basi ikawa ni zamu yake na jamii ya Wakalenjin pamwe na wandani waliomwabudu kujikuza na kusherehekea matunda ya utajiri wa nchi. Mfumo huu wa Moi uliwafanya Wakikuyu kuwa pembezoni mwa ulingo wa kisiasa na uongozi wa kitaifa uliozingatia mtindo wa kuwatunza wazalendo wa utawala huo. Chuki hii iliendelea kuwa mbaya zaidi baada ya Moi shingo upande kukubali kuifanya nchi kuwa na uhuru wa kisiasa mnamo 1992,baada ya kushinikizwa na mashirika ya umma,jumuiya ya kimataifa,watu binafsi kama vile mawakili,waandishi wa habari na wakereketwa wa mapinduzi ya kweli.Mfumo huu aidha uliifanya nchi kuziabudu siasa kwa misingi ya kikabila huku mbegu ya chuki za kikabila iliyopandwa na Kenyatta na Moi ikizidi kuyastawisha matawi yake hadi 2007 ambapo upeo wa athari ulionekana-jamii zikishambuliana zenyewe. Vivo hivo,viongozi tuliyo nao hivi sasa kama vile Kalonzo Musyoka,Uhuru Kenyatta na William Ruto wanaopania kuwania urais mnamo 2012 ni wanafunzi wa kisiasa wa marais waliotangulia na kwa hivyo,mtindo ni ule ule wa 'walimu wao wa kisiasa' utatumika hasa wanaposisitiza kubuni muungano wa kikabila unaowashirikisha Wakikuyu,Wakalenjin na Wakamba. Lakini kama kawaida,tumejitia upofu na kushangilia wanapoturejesha kwenye Jehanamu iwakayo moto lakini tumegubikwa na hamnazo kuu. Manabii wanazidi kubasihri kwamba,litakalotokea litakuwa ni gharika la kisiasa ambalo huenda likawasomba waliobaki,mashamba yao,wana waliozaliwa na damu zao kuzoleka mchangani zisiweze kurudi wala kuonekana tena.Tunajifanya hatujui madhara ya miungano ya kikabila hasa inapovunjika. Damu na roho za waliochinjwa na kuchomwa wakiwa uhai zinazidi kulia katika wafu,huku zikidai na kulilia haki.Haki ya hukumu itendeke kwa wale waliohitimisha mioyo ya wana hawa wa Mungu wasio na makosa hapa duniani kupitia madhila waliyopitia,siku yao ikiwa haijatimia. Haki itendeke kwa wanaotesekea kambini kwa miaka minne sasa huku waliowaua,kuwachinja kama wanyama,kuwabaka na kuwafurusha kutoka mashamba yao wakizidi kuachiliwa kwa ukosefu wa ushahidi. Ndimi za wahanga hawa zimechoka kwa kulilia haki.Sauti zao zimefifia kwa ukosefu wa nguvu ya kulilia haki yao kutokana na njaa,utapiamlo pamwe na baridi shadidi ya usiku ambayo hupenya ndani kwa ndani mle hemani zilizochanikachanika kwa kuangaziwa na jua pamoja na kunyeshewa na mvua kwa muda wa miaka miine. Kipindipindu kimeyachukua maisha yao kutokana na mafuriko yanayowakumba mara kwa mara na kuzisomba hema na kambi zao. Kwa sasa,wamechoka kudai haki kwa kwa manyapaa wasiojali ambao wakati huu wanabuni daraja za kubakia madarakani mnamo 2012,wakiwashajiisha wahanga hawa kuyasahau yaliyopita na kuwaunga mkono katika miungano hii ya kikabila. Na kuonyesha kiwango cha usahaulifu wa kutojali kwa viongozi hawa,wameamua kuzifuja fedha ambazo zingewasitiri wahanga hawa,angaa kuwasahalisha kwa muda njaa,baridi,maradhi na fikra za unyama walioushuhudia ukitendwa dhidi ya wenzao miaka minne iliyopita. Ni mzinduko pekee wa kimawazo,kuzisikiza nyaadhi za manabii wa ukweli zitatunusuru kutoka kwa madhara haya ya ufurukutwa wa ukabila. Hivyo basi,juhudi za Rais Mwai Kibaki kuleta uwiano na maridhiano miongoni mwa Wakikuyu na Wakalenjin mkoani Bonde la Ufa,huenda ukawa na athari za muda mfupi tu kwani unafungamanishwa na kufaulu kumpa upinzani Waziri Mkuu Raila Odinga mnamo 2012,japo makabila haya mawili bado yanaweza yakajitanzua kutoka kwa historia mbaya ya uhasama kati yao.


No comments:

Post a Comment