Monday, 16 July 2012

.

 JOEL GITIMU:WASIFU WA DIWANI MSHAIRI
 
Amewahi kuangaziwa na Taifa Leo mara mbili kama mmoja wa viongozi wachanga zaidi nchini Kenya.Ni kiongozi mshairi,mchanga na mwenye mwonolimwengu mpana.Anaelewa changamoto ambazo wananchi hupitia maanake amedhihirisha wazi kwamba vijana wana uwezo wa kuongoza pasi dhana ambazo huwa na jamii kwamba wao hawafai kutwikwa nyadhifa na wajibu wa uongozi.

Lakini Joel Gitimu,diwani wa wadi ya Lenginet,Nakuru, amedhihirisha kwamba vijana wana uwezo wa kuongoza,na kufikia malengo makubwa ambayo jamii inaweza ikafaidika nao.Tangu aliposhinda uchaguzi mdogo katika wadi hii mnamo 2008,wengi walikuwa na tashwishi kwamba kijana kama huyu angeweza kuwajibikia majukumu sufufu ambayo yalimngojea kama kiongozi aliyetegemewa na jamii kama mfano wa kuigwa.

Nikiwa mkaazi wa wadi hii,ni dhahiri kwamba mengi yamebadilika tangu 2008.Kwanza,eneo hili lina wakaazi wa jamii mbalimbali.Gitimu,chini wa uongozi wake mwenye maono,ameweza kuwaunganisha wakaazi wa hapa pasi kujali jamii wanamotoka.Kupitia kwa ughani wake wa mashairi ambao amekuwa akiufanya katika mikutano ya hadhara,diwani huyu amekuwa katika mstari wa mbele kuupiga vita ukabila na kuwaonya wananchi kwamba ni kikwazo cha ustawi wa kimaendeleo.

Mengi ya mashairi yake huonyesha maudhui ya uzalendo.Aghalabu yeye huwa hatoi hotuba kama wanasiasa wale wengine.

Amekuwa mfano wa kuigwa na vijana,wazee na kila mmoja katika jamii.Chini ya uongozi wake,eneo hili limestawi kimiundo msingi ambayo ilikuwa imedorora hapo kabla.Wanagenzi wa shule za upili wamekuwa wakinufaika kwa fedha za basari ambazo huwasaidia sana wazazi wao katika ulipaji wa karo yao.Mfumo wa utoaji wa fedha hizi aidha umekuwa na uwazi mkubwa,tangu awe diwani.

Badala ya kuita na kuandaa mikutano ya kisiasa,mingi ya mikutano yake huwa ni kumbi za kutoa nasaha kwa wanafunzi hawa kupitia mashairi,hadithi na hotuba zilizojaa na kusheheni nukuu za wanafalsafa mashuhuri.Diwani huyu ni mwandishi mtajika kwani ameandika diwani kadhaa za mashairi,ikiwemo 'Ota na Uwe' iliyozinduliwa miaka miwili iliyopita.Diwani hii imewasaidia wengi katika kuwapa motisha maishani.


Ni dhahiri basi kupitia kwa mfano wa diwani Gitimu,vijana wanao uwezo mkubwa wa uongozi ikiwa wanaweza kupewa nafasi katika jamii kudhihirisha hayo.

No comments:

Post a Comment